Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pengine litapiga kura siku ya Jumanne kuhusu rasimu ya azimio linalotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza ambako wapiganaji wa Hamas na wanajeshi wa Israel wanapambana, shirika la habari la REUTERS limeripoti likinukuu chanzo cha kidiplomasia.
Kura hii itakuja baada ya Marekani kupinga kwa kutumia kura yake ya turuhu azimio kuhusu kusitishwa kwa mapigano huko Gaza siku ya Ijumaa.
Kwa upande mwingine Hamas inasema hakuna mateka atakayeondoka Gaza “hai” bila “mazungumzo”
Hamas imeonya siku ya Jumapili kwamba hakuna mateka hata mmoja waliotekwa nyara wakati wa shambulio la Oktoba 7 na ambao bado wanashikiliwa katika Ukanda wa Gaza atakayeondoka “hai” bila mazungumzo na bila “kukidhi matakwa” yakundi hilo la wanamgambo la Palestina. “Wala adui wa kifashisti na uongozi wake wa kiburi, au wafuasi wake, wataweza kuwaokoa wafungwa wao wakiwa hai bila kufanya mazungumzo, na bila kukidhi matakwa ya Hamas,” Abou Obeida, msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas amesema katika video.