Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Njombe imeendelea kuwa karibu na walipa kodi mkoani humo ikiwemo kutoa misaada kwenye makundi maalumu pamoja na kutoa tuzo kwa wafanyabiashara na taasisi zilizofanya vizuri kwa kulipa kodi.
Miongoni mwa taasisi zilizopata tuzo ni pamoja na kampuni ya Avo africa inayojihusisha na ununuzi pamoja na uchakataji wa zao la Parachichi ambao wamefanikiwa kupata tuzo ya mchangiaji bora wa kodi mwaka 2023.
Awali meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe Specioza Owure amesema katika kipindi cha mwezi Julai wakati wa kuanza mwaka mpya wa fedha wa 2023/2024 wamefikia ufanisi wa zaidi ya asilimia 100 katika makusanyo.
Kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Nahoda Nahoda katika hafla ya utoaji tuzo hizo amesema mchango mkubwa ambao unatolewa na walipa kodi ndio unaofanikisha TRA kufikia malengo ya makusanyo.
Kampuni ya ununuzi Parachichi mkoani Njombe ya Avo Africa chini ya mkurugenzi wake Nagib Karmal imesema imefanikiwa kupata tuzo hiyo kutokana na kufanyakazi hiyo kwa kuzingatia sheria za nchi hususani katika kipengere cha ulipaji kodi.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Njombe Siphael Msigala amewafahamisha wafanyabiashara kusini mwa Tanzania kuwa tayari serikali imeanzisha chombo kitakachosikiliza changamoto za wafanyabiashara pasina kuvuka mipaka.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe ameipongeza TRA kwa kuvuka lengo katika makusanyo yake huku akielekeza weledi kuzingatiwa katika kazi.