Mahakama kuu kanda ya Iringa iliyofanya kikao chake mkoani Njombe imemhukumu kunyongwa hadi kufa Daniel Philipo Mwelango miaka(42),katekista na mkazi wa Makambako baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya Nickson Elias Myamba (43) mkazi wa Makambako mtaa wa Kahawa aliyekuwa katibu wa baraza la walei kanisa Katoliki kigango cha Parokia ya Makambako.
Akisoma hukumu hiyo Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Iringa Said Kalunde amesema mshtakiwa alitekeleza mauaji hayo 8/2/2022 mtaa wa Bwawani katika duka la kanisa Katoliki kigango cha Makambako.
Jaji Kalunde amesema siku ya tukio mshitakiwa alifanya maandalizi kwa kuandaa Panga,Chuma pamoja na mifuko minne ya Kinganjaa,mifuko miwili ilikuwa kwa ajili ya kuzuia damu isisambe na miwili mingine kwa ajili kuhifadhi mwili wa marehemu.
Baada ya hapo akampiga na chuma kwenye kisogo na alipoona ameanguka chini na kufariki alimkata vipande viwili na kuvipaki kwenye mifuko ya kinganjaa ili iwe rahisi kubeba mwili huo kwenda kuutupa mbali,baada ya kuona mke wa marehemu anapiga simu mara kwa mara kwenye simu ya Marehemu pamoja mwenyekiti wa kigango alishindwa kuubeba mwili huo na kuamua kuondoka huku akiwa amelibeba panga na kwenda kulitumbukiza katika shimo la choo cha shule ya msingi Makambako na chuma alichotumia kumpiga nacho alikificha kwenye gata karibu na duka na yeye kutorokea Dar es Saalam.
Aidha Mahakama kupitia upande wa mashtaka imejiridhisha pasina shaka kutokana na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo ambapo Mahakama hiyo imemkuta na hatia ya mauaji kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.