Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amewataka vijana kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na kufanikiwa maishani kwani ukiwa maskini, hakuna atakayekuheshimu.
Shigongo ameyasema hayo katika kongamano la Knowing Youth Purpose lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, lililokuwa na lengo la kuwaongezea vijana uwezo wa kutambua vipawa vilivyomo ndani yao na kuwapa hamasa ya kufukuzia ndoto zao.
Akizungumza na vijana waliohudhuria kongamano hilo, Shigongo aliwataka kutambua kwamba safari ya mafanikio ni ngumu na lazima wajitume kwa nguvu na uwezo wao wote ili baadaye waje kuishi maisha ya ndoto zao.
Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amepitisha mabadiliko ya sheria yanayolenga kuwapa fursa wazawa kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali, tofauti na awali ambapo wageni walikuwa wakipewa kipaumbele kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali, na kuongeza kuwa endapo Watanzania wataitumia fursa hiyo, watajikwamua kiuchumi.
Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, Mtumishi wa Mungu, Mchungaji Timothy Chimeledya pamoja na wageni wengine waalikwa.