Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ametoa maelekezo kwa wakulima wadogo, wakubwa na wanunuzi wote wa chai kuwa chai yote ya Tanzania haitaruhusiwa kuuzwa nje ya utaratibu wa mnada wa Tanzania.
Amesema hayo akiwa ziarani Mkoani Tanga wakati akizindua Kiwanda cha Chai Hai (Organic Tea) cha Sakare kilichopo Bungu. wilayani Korogwe tarehe 13 Desemba 2023.
Mnada wa chai kwa mara ya kwanza ulifanyika jijini Dar es Salaam tarehe 13 Novemba 2023 ambapo kwa kipindi chote huko nyuma Chai ya Tanzania imekuwa ikiuzwa katika mnada wa Mombasa, jambo ambalo limekuwa mwiba kwa wakulima. Chai Ya Tanzania inasifika kwa upekee wa ubora wake (blending) na kwa kutumia mnada wa Mombasa huko nyuma imekuwa haipati bei nzuri na hivyo kuwapunguzia wakulima mapato.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameturuhusu kuanzisha mnada wa chai, ametupatia fedha na kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Serikali itajenga viwanda vingine vitano vya kuchakata chai na kukipanua zaidi kiwanda cha Sakare ili kiweze kuchakata chai nyeusi. Serikali inalenga kuwasaidia wakulima wadogo na kuwapa nafasi wakulima wakubwa kuwa na wigo wa kuzalisha zaidi katika mashamba yao,” alieleza Waziri Bashe. Amepongeza wadau wa maendeleo na watumishi kwa juhudi za kufanikisha mnada huo.