Waziri wa Kilimo, Mhe.Hussein Bashe (Mb) amemwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dkt. Sophia Kashenge kuanza haraka uzalishaji wa miche ya minazi kwa wingi ili wakulima waweze kuipata kwa urahisi.
Amesema hayo akiwa katika Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga tarehe 14 Desemba 2023 wakati akikagua shamba la mbegu la Mwele lililopo chini ya ASA.
Amesema utafiti wa zao la nazi pamoja na ugunduzi wa mbegu bora za zao hilo hufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), hivyo ni vyema sasa kuimarisha mkakati wa upatikanaji wa miche. Waziri Bashe ameongeza kuwa hadi sasa moja ya changamoto kuu katika kuendeleza zao la nazi nchini ni upatikanaji wa miche bora. Ni wakati sasa kuanza kuzalisha kwa wingi ili wakulima waweze kunufaika na zao hilo kibiashara.
Kwa upande wake, Dkt. Sophia amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea shamba hilo na kuweka msukumo mkubwa katika kulifufua baada ya eneo kubwa la shamba kuwa pori kwa zaidi ya miaka 40. Amemhakikishia Mhe Waziri kukutana na TARI ili kuanza kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa.