Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA), Dkt. Sophia Kashenge kuanza mchakato wa kutangaza tenda za ukarabati wa nyumba zote za wafanyakazi, kukarabati ofisi, kukarabati ghala pamoja na kuweka uzio shamba la mbegu Mwele, wilayani Mkinga, Mkoani Tanga.
Amesema hayo tarehe 14 Desemba 2023 wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga katika Shamba hilo la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).
Amesema nyumba zote ambazo zinazotakiwa kufanyiwa ukarabati zitangazwe ili wafanyakazi waweze kuzitumia kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na kuwa karibu shambani.
Waziri Bashe ameelekeza kutangazwe tenda ya kuweka uzio shamba hilo lenye hekta 868 ili kuepuka migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima. Aidha, ameigiza hekta zote 868 za shamba hilo zilimwe ili kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini.
Waziri Bashe amemwambia Dkt. Sophia kuwa aanze kuandaa michoro ya umwagiliaji katika shamba hilo kutokana na kuwepo na mabadiliko ya tabianchi pamoja na maamuzi ya Serikali ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake, Dkt. Sophia Kashenge ameahidi malelekezo hayo ya Serikali yatafanyiwa kazi kulingana na uzito wake. Ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kusimamia kwa karibu na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) hasa katika kuhakikisha uzalishaji wa mbegu unaongezeka.