Mahakama ya kikatiba ya Uganda siku ya Jumatatu ilianza kusikiliza pingamizi la kwanza la sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ambayo imezua ukosoaji kutoka kwa Umoja wa Mataifa na kusababisha vikwazo vya viza vya Marekani kwa maafisa wa serikali.
Taifa hilo la Afrika Mashariki lilipitisha mojawapo ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya ushoga mwezi Mei, hali iliyozusha mtafaruku wa watetezi wa haki na madola ya Magharibi, huku Rais wa Marekani Joe Biden akitishia kupunguza misaada na uwekezaji mjini Kampala.
Lakini serikali ya Rais Yoweri Museveni imekuwa na kauli ya tofauti huku maafisa wakishutumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kuishinikiza Afrika kukubali ushoga.
“Tulikubali kuendelea na mawasilisho yaliyoandikwa kinyume na mawasilisho ya mdomo,” Nicholas Opiyo, wakili anayewakilisha walalamishi, aliambia mahakama mjini Kampala siku ya Jumatatu.
“Mahakama itatoa uamuzi kwa notisi,” naibu jaji mkuu wa Uganda Richard Buteera, ambaye anaongoza jopo la majaji watano katika mahakama ya kikatiba, alisema wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo Jumatatu.
Walalamishi wanaotaka sheria hiyo kubatilishwa ni pamoja na wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu, maprofesa wawili wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala na wabunge wawili wa chama cha Museveni cha National Resistance Movement.
Hakuna tarehe iliyowekwa kwa uamuzi huo.