Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema idadi ya vifo kutokana na mvua kubwa na mafuriko nchini Kenya imeongezeka hadi 174.
Msemaji huyu amewaambia wanahabari mjini Nairobi kuwa licha ya mafuriko kutulia, watu sita wamefariki katika siku tatu zilizopita kutokana na maporomoko ya ardhi yanayohusiana na mafuriko.
Bw. Mwaura amesema kituo cha taifa cha kukabiliana na dharura za El Nino kinaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mafuriko kwa kushirikiana na mashirika husika na mamlaka za mitaa, ili kupunguza athari za matukio haya ya hivi karibuni.
Kulingana na serikali na mashirika ya kibinadamu, mvua kubwa iliyosababishwa na El Nino na mafuriko yameathiri kaunti 38 kati ya 47 tangu Oktoba, na kusababisha mafuriko makubwa ambayo yalisomba nyumba, maeneo yaliyosongwa na maji, ardhi ya kilimo, na kusababisha hasara ya mifugo.
Mwaura alisema kuwa kaunti zilizoathiriwa zaidi na mafuriko ni kaunti za Tana River na Lamu ambazo ziko kusini mashariki mwa nchi ambapo huduma za dharura na misaada zinaendelea.
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imetabiri kuwa mvua kubwa isiyo ya kawaida iliyoanza mwezi wa Oktoba itaendelea hadi Januari 2024.