Samira Sezian raia wa Iran mwenye umri wa miaka 30, aliyefungwa kwa kumuua mumewe, amenyongwa baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela.
Alinyongwa katika gereza la Ghezel Hesar katika mji wa Karaji, Tehran, kwa mujibu wa kundi la Haki za Kibinadamu la Iran (IHR) lenye makao yake Norway.
Kunyongwa kwake kunakuja huku wasiwasi ukiongezeka juu ya idadi ya watu walionyongwa nchini Iran mwaka huu, huku mamia ya watu wakihukumiwa kunyongwa hasa kwa makosa ya dawa za kulevya na mauaji .
Wizara ya Sheria ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba Samira alimuua mumewe kwa makusudi kwa kuchanganya sumu katika vinywaji vyake.
Kulingana na ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Samira aliolewa akiwa na umri mdogo. Nayo ripoti ya Human Rights Watch Foundation, inasema mahakama ilimshtaki kwa kumuua mumewe Januari 2014.
Vyombo vya habari vya ndani nchini Iran viliripoti – familia ya marehemu ilisisitiza kuwa amri ya mahakama hiyo itekelezwe haraka iwezekanavyo.
Na kulingana na BBC Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mauaji nchini Iran mwaka huu, huku takriban watu 115 wakiuawa mwezi Novemba pekee kulingana na Amnesty International.
Kwa mujibu wa IHR, wanawake 18 sasa wamenyongwa nchini Iran mwaka huu, akiwemo Samira. Iran iliwanyonga watu 582 mwaka 2022 lakini mwaka huu idadi inatarajiwa kuwa kubwa zaidi.