Hamas, kundi linalodhibiti Ukanda wa Gaza, limefutilia mbali mchakato wa kuachiliwa tena kwa mateka hadi Israel ikubali “kukomesha kabisa uchokozi”.
Israel inasema imewaua zaidi ya wapiganaji 2,000 wa Hamas huko Gaza tangu kusitishwa kwa amani mapema mwezi huu ambapo mateka zaidi ya 100 waliachiliwa.
Takribani watu 120 waliotekwa nyara kutoka Israel tarehe 7 Oktoba wanaaminika kuwa bado wako mateka huko Gaza.
Juhudi zinaendelea katika Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuhusu vita hivyo.
Marekani imesema bado ina wasi wasi mkubwa kuhusu rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na upigaji kura sasa umeahirishwa hadi Ijumaa.
Mapigano yanaendelea huko Gaza, huku Israel ikishambulia kwa mabomu kaskazini na kusini mwa eneo hilo na Hamas wakirusha makombora mjini Tel Aviv.
Miongoni mwa Wapalestina walioripotiwa kuuawa ni mkurugenzi wa kituo cha polisi katika mji wa kusini wa Khan Younis na binti wa mkuu wa wizara ya afya ya Gaza.
Makubaliano hayo ya wiki moja mwezi huu yalileta ongezeko la misaada katika Gaza, ambapo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba watu wako katika hatari ya kuingia kwenye njaa ikiwa vita kati ya Israel na Hamas vitaendelea.
Mazungumzo kuhusu mapatano mapya yamekuwa yakifanyika mjini Cairo, Misri, ingawa mazungumzo ya awali Jumatano hayakuwa na makubaliano.