Serikali ya Ukraine imepinga tangazo kwamba raia wa Ukraine wanaoishi ng’ambo wataajiriwa kupigana dhidi ya Urusi.
Siku ya Alhamisi, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Rustem Umerov, aliambia chombo cha habari cha Ujerumani Die Welt kwamba wanaweza kuwawekea vikwazo wale wanaokataa kujiunga.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya habari hiyo kutolewa, afisa wa habari wa Wizara, Illarion Pavliuk, alikiambia chombo cha habari cha Ukraine Babel kwamba maoni ya Umerov yametolewa nje ya muktadha.
Pavliuk alidai Waziri wa Ulinzi alikuwa akizungumza kwa ujumla kuhusu jinsi ilivyo muhimu kwa Waukraine – ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi nje ya nchi – kujiunga na jeshi.
Pia alifafanua kuwa kwa sasa hakuna mjadala wowote unaoendelea juu ya kuajiri Waukraine kutoka nje ya nchi.
Mkanganyiko huo unafuatia tangazo la Rais Volodymyr Zelenskyy mapema wiki hii kwamba nchi hiyo inapanga kuhamasisha wanajeshi wapya kati ya 450,000 hadi 500,000.