Kijana mwenye umri wa miaka 18 ambaye alivujisha klipu za mchezo ujao wa Grand Theft Auto (GTA) amehukumiwa kwa agizo la kusalia hospitali kwa muda usiojulikana.
Arion Kurtaj kutoka Oxford, ambaye anakabiliwa na hali ya usonji(Autism), alikuwa mwanachama mkuu wa genge la kimataifa la Lapsus$.
Mashambulizi ya genge hilo dhidi ya makampuni makubwa ya teknolojia ikiwa ni pamoja na Uber, Nvidia na Rockstar Games yaligharimu kampuni hizo karibu dola milioni 10.
Jaji huyo alisema ustadi na hamu ya Kurtaj ya kufanya uhalifu mtandaoni inamaanisha kuwa bado ni hatarini kwa umma.
Ataendelea kuzuiliwa katika hospitali salama maisha yake yote hadi pale madaktari watakapothibitisha kuwa si hatari tena.
Mahakama ilifaamishwa kuwa Kurtaj amekuwa na vurugu akiwa kizuizini huku kukiwa na ripoti kadhaa za majeraha au uharibifu wa mali.
Madaktari walithibitisha kuwa Kurtaj hafai kujibu mashtaka kutokana na ugonjwa wake wa usonji kwa hivyo mahakama iliombwa kubaini kama alitenda au la – si kama alifanya hivyo kwa nia ya uhalifu.
Tathmini ya afya ya akili iliyotumika kama sehemu ya kusikilizwa kwa hukumu ilisema “aliendelea kuonesha nia ya kurudi kwenye uhalifu wa mtandaoni haraka iwezekanavyo. Ana ari kubwa.”
Jaji aliambiwa kuwa alipokuwa kwa dhamana kwa kudukua Nvidia na BT/EE na katika ulinzi wa polisi katika hoteli ya Travelodge, aliendelea kudukua na kutekeleza udukuzi wake mbaya zaidi.
Licha ya kunyang’anywa laptop yake, Kurtaj alifanikiwa kudukua kampuni ya Rockstar, kampuni ya GTA, kwa kutumia Amazon Firestick,Kurtaj aliiba klipu 90 za Grand Theft Auto 6 ambayo haijatolewa na iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu.