Upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, unapinga matokeo ya awali yaliyochapishwa na Tume Huru ya Uchaguzi CENI, katika uchaguzi wa urais ngazi ya diaspora.
CENI imekuwa ikiendelea kuchapisha matokeo hayo ya awali ya uchaguzi wa urais wa Desemba 20.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikiendelea kuchapisha sehemu ya matokeo ya uchaguzi wa urais wa Desemba 20.
Kikao hiki cha kwanza kililenga tu kura ya diaspora ya Congo katika nchi zote tano za kigeni ambapo uchaguzi huu uliandaliwa katika balozi.
Mgombea wa upinzani mfanyabiashara mashuhuri na Gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga Moise Katumbi amepinga matokeo hayo ya awali ya uchaguzi wa diaspora yaliyochapishwa na CENI akiwataka wananchi kutoyakubali.
Kambi za wagombea urais Martin Fayulu na Denis Mukwege zinapanga kuandamana Desemba 27 ili kukemea dosari zilizojitokeza katika maandalizi ya uchaguzi na kutofuatwa sheria ya uchaguzi,
Wagombea hao wanadai kuwa, kura ambayo ilistahili kumalizika kupigwa Desemba 20 inaendelea mpaka sasa.
Waziri wa Mambo ya Ndani na mwanachama wa chama tawala Peter Kazadi amethibitisha kuwa matokeo yaliyochapishwa na CENI ni ya kweli.
”Mchakato wa uchaguzi ulifanyika kwa uwazi, sisi kama serikali hatuna cha kuficha tunataka kuheshimu uamuzi wa raia wa Congo.”