Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amewataka wakazi wa Rombo kuendelea kumpa ushirikiano Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda.
Dkt. Biteko ametoa wito huo hii leo wakati akifunga mashindano ya mbio ndefu ya Rombo na Uchomaji nyama ya Mbuzi yaani ‘Rombo Marathon and Ndafu Festival’ yaliyofanyika hii leo katika eneo la msitu la Rongai,Tarakea wilayani Rombo.
Dkt. Biteko amesema kwamba dhamira ya Prof. Mkenda ya kuanzisha Mashindano na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuchagiza maendeleo ya wilaya hiyo pamoja na uboreshaji wa sekta ya elimu na afya ni jambo la kupongezwa.
“Mbunge yeyote akifanya kazi yake vizuri anachohitaji ni kutiwa moyo na kuombewa, kuna muda hatoonekana Rombo lakini mjue Prof. Mkenda Serikali ilimuona pia anafaa kama ninyi mlivyomuona anafaa hivyo analitumikia taifa katika kuboresha elimu yetu.” Amefafanua Prof. Mkenda
Naibu Waziri Mkuu pia amempongeza Prof. Mkenda kwa maamuzi ya kuita mbio hizo jina la Wilaya Rombo badala ya jina lake binafsi hivyo kuashiria umiliki wa watu wa eneo hilo katika Mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwezi Disemba na kukutanisha wanamichezo kutoka mikoa mbalimbali nchini.
“Huu ni unyenyekevu mkubwa kwa watu wa Rombo, angeweza kuita jambo hili kama Mkenda Marathon na bado tungekuja kushiriki lakini ameanzisha jambo hili na amewaachia wana Rombo kulimiliki na kuliendesha.” Ameeleza Dkt. Biteko.