Wapiga kura wa Tunisia Jumapili wameshiriki kwenye uchaguzi wa kwanza wa wabunge chini ya katiba mpya iliyoshinikizwa mwaka jana na rais Kais Saied.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wapinzani wamesema kwamba zoezi hilo ni hatua ya karibuni zaidi ya kuendeleza ajenda ya udikteta kutoka kwa rais. Saied ambaye alikuwa profesa wa sheria alichaguliwa kuwa rais wa Tunisia 2019, wakati akijitwika madaraka yote miaka miwili baadaye, na kuvunja serikali, pamoja na bunge, huku akitangaza kwamba angetawala kwa kutumia amri ya rais.
Kwenye uchaguzi wa Jumapili, takriban wapiga kura milioni 9 walitarajiwa kuchagua zaidi ya madiwani 2,000 kati ya wagombea 7,000 wanaowania, kulingana na tume huru ya Uchaguzi nchini humo.
Hata hivyo wapinzani wa Saied waliomba wapiga kura kususia, wakitaja zoezi hilo kuwa “kinyume cha sheria” na lenye “ kulazimishwa.”
Mwanahabari mmoja wa AFP kwenye mji mkuu wa Tunis amesema kwamba idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa ndogo, wakati baadhi ya vituo vikibaki tupu kufikia saa za adhuhuri.