Hadi kufikia sasa misaada mbalimbali inayoendelea kutolewa na wadau mbalimbali wilaya ya Hanang’ mkoa wa Manyara palipotokea maafa ya maporomoko ya tope, mawe na magogo ina thamani ya shilingi bilioni 2,583,306,997.00 na fedha taslimu shilingi 5,208,729,711.00.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi katika taarifa yake ya desemba 24, 2023, Fedha taslimu zinajumuisha shilingi bilioni 2.5 zilizoletwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na shilingi 2,708,729,711.00 zilizomo kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kati ya fedha hizo, kiasi cha sh. 2,289,260,025.00 zimechangwa na taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kiasi kilichobaki cha sh. 419,469,152.00 kimechangwa na wahisani mbalimbali.
Serikali inaeendelea kuwashukuru Watanzania kwa utu, upendo, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao umesaidia kupatikana kwa chakula cha kutosha na mahitaji muhimu ili kuwasaidia waathirika kuendelea na maisha yao na kusisitiza wanaoendelea kuleta misaada kujikita zaidi katika vifaa vya ujenzi.
Utaratibu wa kugawa misaada hiyo unaoratibiwa na Idara ya Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na uongozi wa mkoa wa Manyara na wilaya ya Hanang pamoja na kamati zao za usalama, unatumia watalaam kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Kuhusu Mgawo wa misaada , taarifa imeeleza kuwa unalenga kwanza waathirika 1,292 waliothibitika kupoteza nyumba zao ama kuharibika au kuingia tope.
Idadi hii ilipatikana baada ya tathmini ya kina ya picha za satelaiti, rekodi za sensa, ukaguzi halisi wa nyumba hadi nyumba na rekodi za serikali za mitaa katika ngazi ya vitongoji, vijiji na kata.
Utaratibu wa ugawaji misaada umewekwa kwa kubandika majina ya waathirika kwenye ofisi za kata baada ya kukamilika kwa tathmini ambapo mhusika akifika huelekezwa kituo chake cha kupokelea misaada.