Vyombo vya habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), viliripoti Jumatatu, vikinukuu vyanzo vya ndani kwamba watu 20 walifariki katika maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha Jumapili katika jimbo la Kivu Kusini, lililoko mashariki mwanchi hiyo.
Kwa mujibu wa mratibu wa jumuiya ya kiraia katika eneo hilo, Promesse Mazambi, takriban vifo 20 vimeripotiwa katika kijiji cha Kalingi, katika eneo la Mwenga. Mvua hizo pia zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Mwezi Mei 2023, katika eneo la Kalehe katika jimbo la Kivu Kusini, takriban miili 438 ilipatikana katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa. Mamlaka za eneo hilo pia zinakadiria kuwa zaidi ya watu 5,000 wamepotea.
Mafuriko na maporomoko ya udongo ni jambo la kawaida nchini DRC wakati wa msimu wa mvua, ambao huanza Septemba hadi Mei, na mara nyingi huleta madhara makubwa.