Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa wazawa wa Kagera wanaoishi nje ya mkoa pamoja na nje ya nchi ‘Diaspora’ kuja kuwekeza mkoani humo kwani Serikali imeshaweka mazingira wezeshi na rafiki ya Uwekezaji.
Ametoa wito huo leo tarehe 25 Disemba 2023 katika ibada ya Krismasi katika Parokia ya Bikira Maria Mbarikiwa Bushangaro – Nyakaiga, Karagwe mkoani Kagera iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padri Edward Rwechungura pamoja na Padri Georges Kimonges.
“ ‘Diaspora’ pamoja na Majukumu ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuwa katika maeneo mbalimbali ya nchi na mikoani lakini tusisahau kuwekeza nyumbani na niwapongeze Wanakagera wanaoendelea kuwekeza katika mkoa wetu” – amesema Bashungwa.
Waziri Bashungwa amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara nchini ikiwemo mkoa Kagera ambao unaendelea kuunganishwa na nchi jirani kwa ujenzi wa barabara za lami.
“Kwa mfano kwetu sisi ukanda wa Bushangaro, mawasiliano ya barabara hayakuwa mazuri lakini barabara zinazidi kuboreshwa na ‘Diaspora’ mnapokuja mmekuwa mkinipigia kunieleza mambo yalivyobadilika” – amesema Bashungwa