Wanachama wasiopungua 80 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameuawa katika operesheni ya Jeshi la Taifa la Somalia katika mkoa wa Mudug, kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hayo yalisemwa jana Jumanne na Brigedia Jenerali Dayah Abdi Abdulle, Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Somalia ambaye ameeleza kuwa, wanamgambo hao waliuawa katika operesheni kabambe iliyofanywa na wanajeshi wa Somalia katika msitu mmoja ulio karibu na mji wa Caad, jimboni Mudug.
Brigedia Jenerali Abdulle amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, operesheni dhidi ya genge hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda inaendelea.
Haya yanajiri siku mbili baada ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia kutangaza kuwa, magaidi wasiopungua 130 wa kundi hilo la wanamgambo wameangamizwa katika mapigano baina yao na jeshi la Somalia katikati mwa majimbo ya Hir Shabelle na Jubaland, kusini mwa nchi.
Aidha jeshi la Somalia lilinasa silaha na zana kadhaa za kivita kutoka katika maficho ya magaidi wa al-Shabaab kwenye operesheni hizo za kulitokomeza genge hilo.