Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewaasa watanzania kuhakikisha wanakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo kwa kuwa ardhi iliyopo haiongezeki na idadi ya watu inazidi kuongezeka.
Mhe. Pinda amesema hayo tarehe 26 Desemba 2023 nyumbani kwake Kibaoni, Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi katika hafla maalum ya chakula aliyowaandalia wananchi na viongozi wa jimbo lake kusheherekea Siku Kuu ya Chrismas.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, Naibu Waziri huyo wa Ardhi alisema, wakati serikali ikiandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, watanzania wanatakiwa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi huku wakielewa changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kuwa ardhi haiongezeki.
‘’Miaka 25 inayokuja lazima tufikirie hizi hekta na ekari tulizopopewa na Mungu ikaitwa Tanzania inatushoje itakapofika miaka hamsini ijayo, kwa hiyo ni sisi ndiyo tutakaopanga tutumiaje maeneo yetu’’ alisema Mhe. Pinda.
‘’Kila mtu akikaa ajue ardhi ni yake na ndugu zake kwa hiyo tuishi kwa amani na tusigombane, hakuna namna tutakachokifanya katika eneo hili ni lazima tukubaliane namna ya kuitumia ardhi ndogo katika ongezeko kubwa la watu’’. Alisema Pinda