Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alisema siku ya Jumatano kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hana tofauti na Adolf Hitler na alifananisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na kuwatendea Wayahudi na Wanazi.
Mwanachama wa NATO Uturuki, ambayo inaunga mkono suluhu la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina, imekosoa mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel dhidi ya Gaza, na kuyataja kuwa ni “nchi ya kigaidi” na kusema viongozi wake lazima wahukumiwe katika mahakama za kimataifa.
Akizidisha matamshi yake, Erdogan alisema Uturuki itawakaribisha wasomi na wanasayansi wanaokabiliwa na mateso kwa maoni yao kuhusu mzozo wa Gaza, akiongeza kuwa nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Israel zinahusika katika kile alichokiita uhalifu wa kivita.
“Walikuwa wakimsema vibaya Hitler. Wewe una tofauti gani na Hitler? Watatufanya tumkose Hitler. Je, anachofanya Netanyahu ni kidogo kuliko kile Hitler alifanya? Sivyo,” Erdogan alisema.
“Yeye ni tajiri kuliko Hitler, anapata uungwaji mkono kutoka nchi za Magharibi. Kila aina ya usaidizi unatoka Marekani. Na walifanya nini kwa msaada huu wote? Waliua zaidi ya Wagaza 20,000,” alisema.
Netanyahu alijibu kwa kusema rais wa Uturuki anafaa kuwa mtu wa mwisho kuhutubia Israel.
“Erdogan, ambaye anafanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wakurdi, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya kuwafunga waandishi wa habari wanaopinga utawala wake,” Netanyahu alisema katika taarifa yake, “ni mtu wa mwisho ambaye anaweza kutuhubiria maadili.”
Licha ya ukosoaji wake dhidi ya Israel, Uturuki imedumisha uhusiano wa kibiashara na hivyo kuibua upinzani kutoka kwa vyama vya upinzani na Iran. Ankara inasema biashara na Israel imeshuka kwa kiwango kikubwa tangu Oktoba 7, wakati kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas lilipoanzisha mashambulizi makali ya kuvuka mpaka na kuua watu 1,200, na kuifanya Israel kuanzisha vita vyake dhidi ya Hamas.
Tofauti na washirika wake wa Magharibi na baadhi ya mataifa ya Kiarabu, Uturuki haioni Hamas kama shirika la kigaidi.