Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema linahitaji jumla ya dola za Kimarekani milioni 364 katika shughuli zake zote ili kuongeza msaada wa kibinadamu nchini Somalia kati ya Disemba 2023 na Mei 2024.
Hayo yamo kwenye ripoti mpya ya WFP iliyotolewa Jumanne usiku, ambayo inabainisha kuwa kati ya kiasi hicho, fedha za dharura za misaada ya kibinadamu na lishe ya kuokoa maisha ni dola milioni 315.5. Mwaka 2023, inakadiriwa kuwa watoto milioni 1.5 walio chini ya umri wa miaka mitano wamepata utapiamlo mkali, huku watoto 331,000 wakikabiliwa na utapiamlo unaotishia maisha.
Kwa mujibu wa WFP, wakati Somalia bado inakabiliwa na athari za ukame, kuanza kwa mafuriko yaliyosababishwa na El Nino kuliongeza mzigo wa jamii zilizo karibu na mito ya Juba na Shabelle kusini mwa Somalia, na kusababisha madhara makubwa katika jamii nyingi.
Nalo Shirika la Kukabiliana na Majanga la Somalia linasema watu milioni 2.4 wameathiriwa na mvua kubwa na mafuriko, huku milioni 1.2 wakilazimika kuyahama makazi yao na watu 118 wakipoteza maisha.