Mamlaka ya Zambia ilitangaza siku ya Alhamisi kuwa wanaongeza kampeni yao ya afya kukabiliana na kipindupindu, ugonjwa ambao umekuwa ukiongezeka tangu Oktoba na tayari umeshagharimu maisha ya karibu watu mia moja katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika mwaka huu.
Waziri wa Afya, Sylvia Masebo, alitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali zaidi za usafi katika kaya, na mwenzake anayeshughulikia Maji, Mike Mposha, alisema kuwa klorini itasambazwa kwa wingi ili kuzuia maji machafu katika mikoa iliyoathiriwa zaidi na kipindupindu.
Vifo vitano na visa vipya 111 vya maambukizi vilirekodiwa ndani ya saa 24, hasa kutokana na mvua kubwa, ambayo huharakisha maambukizi ya ugonjwa wa bakteria kupitia maji na chakula kilichoambukizwa, alisema Sylvia Masebo. Hii ndio jumla ya juu zaidi ya kila siku katika 2023.
Kumekuwa na vifo 93 mwaka huu kutokana na maambukizo haya ya papo hapo ya kuhara, wengi tangu Oktoba, kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma.
“Taifa letu linakabiliwa na changamoto kubwa ya kiafya,” Bi Masebo aliambia mkutano na wanahabari. Kiwango cha vifo vya janga la sasa, karibu 3%, “inatia wasiwasi sana”, aliongeza, akikumbuka kuwa kimataifa, ni chini ya 1%.
Zimbabwe, jirani wa Zambia pia aliyeathiriwa na kipindupindu, imetangaza hali ya hatari. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya vifo 250 vimerekodiwa tangu Februari.
WHO imeelezea wasiwasi wake kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa kipindupindu duniani katika miaka ya hivi karibuni, huku Afrika ikiwa imeathirika zaidi.
Idadi ya wagonjwa wa kipindupindu walioripotiwa imeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka 223,370 mwaka 2021 hadi 472,697 mwaka 2022.