Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 kwa sasa umefikia asilimia 94.78 huku mashine mbili za kuzalisha umeme zikiwa tayari zimeshafungwa kwa ajili ya kuanza kuzalisha umeme.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 28 Desemba 2023 wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi huo wilayani Rufiji akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati aliyoteua Rais ya ufuatiliaji mradi wa JNHPP, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.
” Hatua iliyopigwa ya utekelezaji wa mradi huu kila mtu ameona kuwa ni kubwa kwenye hatua zote, mfano kwenye ujazaji maji wa bwawa la kuzalisha umeme, maji yamejaa kwa kiwango ambacho yanaruhusu kuzalisha umeme, pia ufungaji wa mashine ambazo zitatumika kuzalisha umeme, nafurahi kusema kuwa mashine mbili zimeshafungwa ambazo ni mashine namba Tisa na namba Nane na tunaamini kwamba mashine nyingine zitaendelea kufungwa kadri muda unavyoenda ili kupata megawati zote 2,115.” Amesema Dkt. Biteko