Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema wapenzi wa jinsi moja nchini Burundi “wanapaswa kupigwa mawe” na kwamba hiyo haitakuwa uhalifu.
Rais alisema hayo katika mkutano wa moja kwa moja na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, akijibu swali la mwandishi wa habari. Alisema kuwa nchi zenye nguvu “zinapaswa kusalia” na misaada yao kwa Burundi ikiwa misaada hiyo inaambatana na wajibu wa kutoa haki kwa wapenzi wa jinsi moja.
Alitumia maandiko ya biblia kusema kwamba Mungu anachukia mapenzi ya jinsi na kusema kwamba suala hilo halina mjadala nchini Burundi.
“Kwangu mimi, nadhani ikiwa tutapata watu hawa nchini Burundi wanapaswa kupelekwa kwenye viwanja vya michezo na kupigwa mawe, na kufanya hivyo haitakuwa kosa,” rais alisema.
Bw Ndayishimiye alisema uhusiano wa jinsia moja ni kama “kuchagua kati ya Shetani na Mungu”.
“Ikiwa unataka kumchagua Shetani sasa nenda ukaishi katika nchi hizo, na nadhani wale wanaojitahidi kwenda huko wanataka kuiga tabia hizo, wanapaswa kubaki huko na kamwe wasituletee,” rais aliongeza.
Mapenzi ya jinsi moja ni kinyume cha sheria nchini Burundi na adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka miwili jela.