Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko leo tarehe 29 Disemba, 2023 amezindua Zahanati ya Bungoni iliyopo mtaa wa Mafuriko Ilala jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa huduma ya zahanati hiyo kutumia huduma badala ya kwenda mbali kufuata huduma za Afya, kwani ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.
“Niwaombe viongozi wenzangu tuliopewa dhamana na Mhe. Rais kuhakikisha tunawahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge kwa kuwapatia huduma bora wanazostahili.” Alisisitiza Dkt. Biteko
Aliwataka wananchi wa Ilala kumpa ushirikiano Mbunge wao kwa vitendo na kumpongeza kwa kazi kubwa aliyofanya ya kuleta Maendeleo kwa wanachi wake, na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wa Mbunge huyo kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo na kukemea wachache wanaojificha kwenye kivuli cha taratibu kuchelewesha maendeleo.
Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwezi februari mwaka huu, kwa jitihada za wananchi na baadae Serikali na umegharimu kiasi cha shilingi milioni 351, ukihusisha gharama za ujenzi, samani, dawa na vifaa tiba na umefadhiliwa na African Relief Agency na Taasisi ya Rahma International kutoka Kuwait na inamilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali.
Aidha, Dkt. Biteko alipata fursa ya kutembelea jengo hilo linalohusisha wagonjwa wa nje yani OPD, Kliniki ya Baba, Mama na Mtoto pamoja na jengo la kujifungulia na kusalimiana na kinamama waliojifungua kwenye Zahanati hiyo.
Zahanati hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia kata nne zilizopo wilaya ya Ilala ambazo ni Ilala, Buguruni, Sharifu Shamba, na Mchikichini wapatao Elfu 12.