Mahakama ya Juu ya Senegal imethibitisha hukumu iliyotolewa Mei mwaka jana na Mahakama ya Rufaa ya kifungo cha miezi sita jela dhidii ya kinara wa upinzani nchini humo, Ousmane Sonko, kwa kumkashifu Waziri wa Utalii, Mame Mbaye Niang.
Mpinzani huyo sasa hataweza kugombea katika uchaguzi wa rais mwezi ujao, licha ya kwamba wanasheria wake wanaendelea kuwa na matumaini ya kukata rufaa.
Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Senegal umetolewa usiku wa kuamkia leo, muda mfupi kabla ya saa sita usiku Alkhamisi, baada ya takriban saa 12 za kusikilizwa ambapo mawakili wa pande zote mbili walibishana kwa muda mrefu kwa ajili ya wateja wao, ambao hawakuwepo mahakamani.
Ousmane Sonko amehukumiwa baada ya kukata rufaa ya kifungo cha miezi sita jela kwa kumtusi na kumtuhumu hadharani Mame Mbaye Niang, Waziri wa sasa wa Utalii kuwa amehusika na ubadhirifu.
Sonko ambaye ni kiongozi wa chama cha PASTEF, mwenye umri wa miaka 49, alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2019, na alihukumiwa mnamo mwezi Machi 2023 katika mahakama ya mwanzo kifungo cha miezi miwili jela, na kutakiwa kulipa faranga za CFA milioni 200 (karibu. 300,000 euro) kama fidia.
Mwezi Julai mwaka jana pia Ousmane Sonko alishtakiwa kwa kupanga uasi na makosa mengine kadhaa.