Klabu ya Mchezo wa Riadha ya Goba Roads Runners (GRR) leo imetangaza rasmi uzinduzi wa mbio za Goba Hills Marathon (GHM) kwa Mwaka 2023 ambazo zitakuwa zikifanyika kwa mwaka wa tano mfululizo baada ya mafanikio ya misimu minne kuanzia zilipoanza rasmi mwaka 2020.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika mnamo tarehe 3 Februari 2023 kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Goba wilayani Ubungo Jijini Dar Es Salaam.
Kauli mbiu ya Goba Hills Marathon 2024 ikiwa ni “Kimbia, Okoa Maisha ya Mama na Mtoto” ambapo lengo kuu la mbio hizo ni kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kuboresha mazingira ya hospitali hasahasa wodi zakujifungulia za akina mama.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa kutangaza mbio hizo na kuzindua jezi rasmi zitakazotumika pamoja na medali za washiriki wa mbio hizo, Mwenyekiti wa Klabu ya Goba Roads Runners (GRR) Revocatus Kahendaguza kuwa klabu inajivunia kuendesha mbio za Goba Hills Marathon kwa mafanikio makubwa kwa misimu mitano mfululizo ikiwa ndio klabu ya kwanza ya mbio nchini kuendesha Marathon ya kiwango cha kisasa na kugusa jamii inayowazunguka moja kwa moja.
“Tunayo furaha kubwa kwani unapoongelea mchezo wa riadha nchini huwezi kuacha kutaja mchango wa klabu yetu ambayo inaendeshwa kwa mfumo wa wanachama. Klabu imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha jamii kuishi misingi ya afya bora ambayo ni kipaumbele cha taifa.
Nia yetu ni kuendelea kuifikia jamii kubwa zaidi kupitia elimu na kufanya matukio mengi zaidi ya mchezo wa riadha”.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu, Bw. Benson Luoga alisema kwamba klabu itatoa asilimia 10% ya mapato ya mbio hii kwa ajili ya kugusa jamii katika eneo la Mama na Mtoto kama ilivyokuwa katika misimu minne iliyopita ambapo klabu iliweza kuchangia vifaa tiba mbali mbali vya mama na mtoto katika zahanati ya Goba, iliyopo Ubungo jijini Dar Es Salaam.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Klabu na Mwandaaji wa Goba Hills Marathon, Similwa Mdumbwa alisema kuwa mbio hizo zitakuwa za kilomita 42.2 (Full Marathon), 21.1 kilometa (Half Marathon), kilomita 10 (Corporate Run) na kilomita 5 (Family Run).
Bw. Mdumbwa alisema usajili kwa ajili ya kushiriki mbio hizo kuwa ni Tsh. 35,000 kwa kila mbio na tayari usajili umeshafunguliwa na washiriki wameanza kujisajili. Kwa vikundi au taasisi gharama ya kujisajili ni Shilingi 30,000 kuanzia watu 10 na kuendelea. Aliongeza kuwa
“Tayari jezi za washiriki wa mbio ya Goba Hills Marathon pamoja na medali za watakaomaliza zimekwishafika nchini na leo tunazizindua rasmi hapa, hivyo washiriki wasitarajie longo longo kama ambazo zimewahi kujitokeza kwenye baadhi ya mbio nchini ambapo wanajisajili kisha vifaa muhimu vya mbio havijafika”. Goba Roads Runners (GRR) ni klabu ya michezo inayotambulika na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kama waandaaji na washiriki wazuri kwenye mchezo wa riadha Tanzania.