Tetemeko kubwa la ardhi lililotikisa katikati mwa Japani mnamo Januari 1 lilisababisha vifo vya watu 161, wakati watu 103 bado hawajulikani walipo, kulingana na hesabu mpya iliyotangazwa Jumatatu asubuhi na viongozi wa eneo hilo.
Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.5 kwenye kipimo cha Richter pia lilisababisha watu 560 kujeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la Ishikawa, ambalo ndilo lililoathiriwa zaidi na maafa hayo.
Tetemeko hilo la ardhi, lililofuatwa na mamia ya mitetemeko ya baadaye, lilisababisha kuporomoka kwa majengo na barabara, na pia lilisababisha Tsunami, mawimbi ya urefu wa zaidi ya mita yakigonga kwenye ufuo wa rasi ya Noto, ukanda mwembamba wa ardhi wenye urefu wa kilomita mia moja unaosambaa ndani Bahari ya Japan.
Tetemeko hilo lilisikika hadi Tokyo, umbali wa kilomita 300.
Maelfu ya waokoaji kutoka kote nchini Japani, ambao wanaendelea kuchunguza vifusi wakitafuta miili, lazima wakabiliane na theluji iliyoanguka kwenye rasi ya Noto siku ya Jumatatu.
Maporomoko mapya ya ardhi kutokana na mvua yanahofiwa na hali ya barafu inatarajiwa kutatiza zaidi shughuli kwenye barabara zilizoharibiwa na tetemeko hilo, mamlaka imeonya.