Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa kauli za chuki zenye misingi ya kikabiila na uchochezi wa ghasia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumapili jijini Geneva Uswisi Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa UN amezungumzia kuongezeka kwa kauli hizo hasa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini na pia katika mikoa ya Kasaï na Katanga, baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita.
“Kauli za chuki, za kudhalilisha utu na za uchochezi ni za kuchukiza na zinaweza tu kuongeza mvutano na vurugu katika nchi ya DRC yenyewe, pamoja na kuweka hatarini usalama wa kikandari,” amesema Kamishna Türk.
Ameeleza kutambua juhudi za baadhi ya mamlaka za Kongo DR dhidi ya tabia hiyo, lakini amesisitiza kuwa hatua kali zaidi zinahitajika kuchukuliwa.
“Natoa wito kwa mamlaka kuchunguza kwa kina na kwa uwazi ripoti zote za kauli za chuki na uchochezi wa vurugu na kuwawajibisha waliohusika,”amesisitiza Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.