Mahakama ya Juu nchini India leo imeufuta msamaha uliotolewa kwa wanaume 11 wa kihindu ambao walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumbaka kwa zamu mwanamke mmoja muislamu na kuwauwa ndugu zake.
Uhalifu huo ulimefanyika wakati wa ghasia za kidini zilizolitikisa jimbo la Gujarat zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Kwenye mkasa huo wa mwaka 2002 uliotokea katikati ya mapambano baina ya jamii za wahindu na waislamu, wanaume hao walimbaka kwa zamu Bilkis Bano, aliyekuwa wakati huo mjamzito na kisha kuwauwa ndugu zake 7 ikiwemo mtoto wake wa miaka mitatu.
“Ombi lao la kulindwa uhuru wao limekataliwa,” mahakama ilisema. “Kuwaweka nje hakutakuwa kwa kuzingatia utawala wa sheria.”
Bano, ambaye sasa ana umri wa miaka 40, alikuwa na ujauzito wa miezi mitano alipobakwa na genge wakati wa ghasia, ambazo zilishuhudia karibu watu 2,000, wengi wao wakiwa Waislamu, wakiuawa katika baadhi ya machafuko mabaya zaidi ya kidini ambayo India imewahi kukumbana nayo.
Watu saba kati ya 14 waliouawa katika tukio moja walikuwa jamaa wa Bano, akiwemo binti yake mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye kichwa chake kilivunjwa ardhini na wahalifu katika wilaya ya Dahod ya Gujarat.
Katika uamuzi wake wa leo, Mahakama ya Juu imeamuru wanaume hao wajisalimishe mara moja gerezani ndani ya muda wa wiki mbili zinazokuja.