Mahakama ya Kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatazamiwa kuanza kusikiliza kesi ya kupinga uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita.
Ombi la kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais liliwasilishwa wiki iliyopita na Théodore Ngoy, ambaye alikuwa wa mwisho katika uchaguzi huo.
Aliyataja matokeo hayo kuwa ni “uzushi”.
Wagombea wawili wakuu wa upinzani, Moïse Katumbi na Martin Fayulu, walipinga matokeo lakini walikataa kuyapinga mahakamani.
Mahakama ya Kikatiba inatarajiwa kutoa uamuzi kabla ya Januari 12, wakati bodi ya uchaguzi itakapotangaza matokeo ya mwisho.
Ikiwa ombi la Bw Ngoy litatupiliwa mbali, Rais Felix Tshisekedi ataapishwa kwa muhula wa pili Januari 20, baada ya kushinda uchaguzi kwa asilimia 73 ya kura.
Uchaguzi wa Desemba 20 ulikumbwa na matatizo mengi ya vifaa Ilibidi kurefushwa kwa hadi siku ya pili katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo kubwa.
Siku ya Jumamosi, bodi ya uchaguzi iliwafutia uchaguzi wagombea 82 wa ubunge, majimbo na mitaa, kwa sababu ya udanganyifu na ghasia.