Korea Kusini imepiga kura kupiga marufuku nyama ya mbwa na kumaliza utata kuhusu desturi hiyo ya zamani, huku wanakampeni wakiita “historia inayoendelea”.
Hadi mbwa milioni moja hufugwa na kuuawa nchini Korea Kusini kila mwaka, lakini mitazamo imebadilika katika siku za hivi majuzi na mahitaji ni ya chini sana.
Marufuku hiyo itafanya ufugaji, uchinjaji na uuzaji wa mbwa na nyama ya mbwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu kuwa kinyume cha sheria kuanzia 2027, pamoja na adhabu ya hadi miaka mitatu jela au faini ya hadi KRW 30m (£18,000).
Kuanzisha mashamba mapya ya mbwa, vichinjio na vifaa vya kupikia na usindikaji vitapigwa marufuku mara moja.
Bunge la Korea Kusini liliidhinisha mswada huo wa kihistoria kwa kura 208 dhidi ya sifuri siku ya Jumanne, lakini baadhi ya wafugaji wa mbwa walisema walipanga kukata rufaa na maandamano.
Kula nyama ya mbwa ni tabia ya karne nyingi nchini, hata hivyo tafiti zinaonyesha watu wengi hawatumii tena.