Tumaini Luvanda (35) mkazi wa Dombwela wilaya ya Makete mkoani Njombe ameuawa kwa kukatwa na panga vipande kisha kutenganishwa kichwa na kiwiliwili na baadhi ya viungo kutupwa kwenye mto jirani na nyumbani katika eneo la Kabinda wilayani humo ambapo tayari Polisi inamshikilia Juma Kyando (36) ambaye ni mume wa Tumaini (Marehemu) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Iwawa ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa wa Dombwela Joseph Mbilinyi amesema tukio limetokea usiku wa kuamkia January 8,2024 ambapo alifika nyumbani kwa mtuhumiwa mara baada ya kupigiwa simu na majirani na kumkuta Kyando akiwa na Panga jambo lililomfanya apige simu Polisi ili kuomba msaada.
“Baada ya Polisi kuja alikuwa ameshamuua mkewe na kumuweka kwenye mfuko wa kisarufeti na kwenda kutupa kwenye mto,kwenye uwanja wake tuliuona Moyo wa mwanadamu ndio tukaanza kufuata kwenye mto kwasababu alikuwa anavuta sarufeti lakini kufika kwenye mto tukaona kisarufeti kinaelea kwenye maji tukakiopoa na kuendelea kufuata tena mto tukakiona kiungo kingine ambacho ni ubavu upande wa titi na shingo nacho tukakiopoa tukaanza kutafuta kichwa ambacho kimetusumbua kwa muda mrefu”amesema Mwenyekiti
Mkuu wa Polisi wilaya ya Makete mrakibu mwandamizi wa Polisi Assel Mwampamba amesema tukio hilo si la kawaida na kutoa ushauri kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuwa na namba za jeshi la Polisi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza “Hili lingezuilika sasa ametoka na Panga mkakimbia wote na wanaume acheni uwoga yaani mtu yuko mmoja anacharanga mtu ninyi mmekimbia mngekuwa mnamrushia mawe asingeendelea kukata mtu pale”
Kwa upande Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Njombe Mrakibu wa Polisi Joseph Malongo akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe mara baada ya kufika eneo la tukio amesema kuwa ni lazima mtuhumiwa aweze kuchukuliwa sheria “Niwape pole kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe,mwenzetu bwana Juma amejichukulia sheria mkononi jeshi la Polisi lazima tumchukulie hatua stahiki na tumpeleke Mahakamani haraka iwezekanavyo”
Medrick Kyando ni ndugu wa Mtuhumiwa wa mauaji ya mkewe pamoja na baadhi ya majirani wamesema Kyando ni fundi wa kujenga alikuwa hana makundi pia hana historia ya kuwa na matatizo ya akili na alikuwa anaishi vizuri na mke wake lakini wanashangaa kuona ametekeleza tukio hilo la kikatili lililowashtua ambapo kwa sasa anaacha watoto wadogo watatu akienda Polisi na mkewe akiwa amefariki.