Mahakama nchini Sierra Leone imewashtaki wanajeshi 27 kwa madai ya jaribio la mapinduzi.
“Mashtaka hayo ni pamoja na uasi, kushindwa kukandamiza uasi, mauaji, kusaidia adui, kuwasiliana na adui na makosa mengine yanayohusika,” wizara ya ulinzi ilisema katika taarifa yake.
Novemba mwaka jana, watu wenye silaha walivamia ghala la kijeshi na magereza kadhaa mjini Freetown, na kuwaachilia karibu wafungwa 2,000.
Mamlaka ilielezea hatua hiyo kama jaribio la “kupindua” serikali.
Wiki iliyopita, Rais wa zamani Ernest Bai Koroma alishtakiwa kwa uhaini kuhusiana na tukio hilo hilo.
Alikanusha kuhusika kwa vyovyote katika matukio ambayo watu 20 waliuawa.
Mamlaka pia inamfungulia mashtaka mmoja wa walinzi wa rais wa zamani wa Bw Koroma pamoja na polisi 11 wa zamani na maafisa wa magereza.
Wameshutumiwa kwa uhaini, kuficha uhaini na “kuhifadhi, kumuelekeza na kumsaidia adui”.
Ghasia za mwezi Novemba zilikuja miezi mitano baada ya uchaguzi ambao ulishuhudia Rais wa sasa Julius Maada Bio kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.
Matokeo hayo yalikataliwa na upinzani na kukosolewa na waangalizi wa kimataifa kwa ukosefu wa uwazi.