Mwanamke kutokea nchini Uingereza amefariki dunia siku chache tu baada ya upasuaji wa kuongeza shepu ama (BBL) nchini Uturuki, kwa mujibu wa gazeti la The Sun. Demi Agoglia, (26) kutoka jiji la Manchester alipata mshtuko wa moyo masaa machache kabla ya kuondoka kuelekea Uingereza kutokea Uturuki.
Kulingana na maelezo ya familia yake, alipatwa na mshtuko wa moyo akiwa njiani kuelekea hospitali jijini Istanbul kufanyiwa uchunguzi baada ya upasuaji huo unaojulikana kama BBL.
Mume wake Agoglia Bradley Jones alimpatia huduma ya dharura ya CPR kabla ya kukimbizwa hospitalini lakini madaktari hawakuweza kumuokoa, kulingana na gazeti la The Sun.
Kiwango cha kifo kinachotokana na upasuaji wa kuongeza makalio (BBL) ni mtu mmoja kati ya kila watu 3000, ikiwa ndio upasuaji wenye kiwango cha juu zaidi cha vifo vilivyorekodiwa kuliko upasuaji mwingine wowote wa urembo.
Inaaminika kuwa Agoglia alipatwa na mshtuko wa moyo kutokana na mshipa wa mafuta, ingawa aliambiwa upasuaji wake ulikuwa wenye mafanikio. Mwanadada huyo alijifungua mtoto wake wa mwisho miezi saba iliyopita na alikuwa amesafiri kwa ndege hadi Uturuki kwa ajili ya upasuaji huo.