Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa mapigano ya kijeshi nchini Sudan yanasababisha idadi kubwa ya watu kukimbia makazi yao duniani na kuvuruga mapambano dhidi ya mlipuko hatari wa kipindupindu.
Ofisi hiyo ina wasiwasi mkubwa na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan kutokana na kuenea kwa mzozo, ambao umechochea msukosuko mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani. Tangu mwezi Aprili, watu zaidi ya milioni 6 wamekimbia makazi yao nchini humo, wakiwemo watu zaidi ya laki 5 kutokana na mapigano yaliyozuka katika Jimbo la Aj Jazirah mwezi uliopita.
Wasaidizi hao wa kibinadamu wamesema kuwa wengine zaidi ya milioni 1.3 walikimbia na kuvuka mipaka ya Sudan na kuwa wakimbizi katika nchi jirani za Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.