Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mark Mulwambo amesema pamoja na ofisi hiyo kutambua umuhimu wa watumishi wake, amewataka waendelee kuzingatia uadilifu na usiri katika kutenda kazi zao.
Alisema hayo mjini Morogoro wakati wa mafunzo elekezi juu ya Mfumo wa usajili wa mashauri ya Mahakama kuu ya Tanzania (e-CMS) na utunzaji wa nyaraka za serikali kwa watumishi wa kada ofisi hiyo ya wakili mkuu wa serikali.
Mulwambwo alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa serikali kwenye kada mbalimbali nchini kuvujisha nyaraka za serikali na kuonekana zikichambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kinyume cha sheria na taratibu
Aidha alisema chanzo cha kuvuja kwa nyaraka za serikali mara nyingi huwa ni ama watumishi walipewa dhamana ya kuzitunza kutokuwa makini ama kuzivujisha kwa makusudi kwa maslahi yao binafsi.
“Niwasihii kuwa makini na kutumia ujuzi wenu katika mafunzo hayo kuondoa hali hiyo ya kuvuja nyaraka za serikali, sitarajii kuona mtumishi tena aliyepata mafunzo anakuja kuwa katika tuhuma za uvujishajii wa nyaraka hizo, na hiyo ni njia ya kuepuka madhara ya kufanya hivyo,”alisema.
Mulwambwo alisema serikali haitakuwa na muamana na mtumishi atakayebainika kuhusika na uvujishaji wa taarifa zake za aina yoyote.
Pia alisema katika kipindi cha mwaka 2023 ofisi ya wakili mkuu wa Serikali kupitia kitengo cha masjala ya sheria imeweza kufanya mambo mbalimbali ikiwemo upokeaji wa nyaraka za malalamiko na mawasiliano ya sheria, kupokea na kusajili mashauri yote yanayofunguliwa dhidi ya serikali na kutunza taarifa kwenye mfumo wan CIMS, kufuatilia na kuratibu Causelist za mahakama na mabaraza ya maamuzi na usuluhishi, kuandaa ushaidi wa migogoro ya usuluhishi.
Kaimu naibu huyo alisema mafunzo hayo ni ya kujitathimini utendaji wa kazi na kupata fursa ya kukumbushwa miiko na taratibu za kiutendaji hasa katika usiri na utunzaji wa nyaraka za Serikali kwa njia ya Kielektroniki.