Raia wa visiwa vya Comoro watapiga kura kesho kumchagua rais na wabunge, kwenye uchaguzi ambao wanasiasa wakuu wa upinzani wamewaambia wafuasi wake waususie.
Kampeni zilimalizika siku ya Ijumaa na sasa wapiga kura wapatao 340,000 wakitarajiwa kupiga kura kwenye nchi hiyo yenye watu chini ya Milioni moja.
Rais Azali Assoumani, anatarajiwa kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi huu, ambao umewaacha wapinzani wakiwa wamegawanyika.
Baadhi ya wanasiasa wakuu wameawaambia raia wa Comoro wasishiriki uchaguzi huo ambao rais Assoumani, anakabiliwa na wapinzani wengine watano.
Wanasiasa hao wanasema, uchaguzi huo hauwezi kuwa huru na haki kutokana na mchakato wa kampeni kuvurugwa na Tume ya Uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi wa Jumapili, yanatarajiwa kutangazwa baada ya siku chache zijazo, na iwapo hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja, atakayepata asilimia 50 ya kura, kutakuwa na duru ya pili tarehe 25 mwezi Februari.