Waasi wa Houthi nchini Yemen, wameapa kulipiza kisasi baada ya Marekani na Uingereza kuwashambulia katika ngome zao, kwa kuyumbisha usalama kwenye Bahari ya Shamu.
Uongozi wa waasi hao, umetaja kushambuliwa kwa wapiganaji wake kama kitendo cha kihalifu na kuapa kuendelea kulenga meli zinazopitia kwenye Bahari hiyo kwenda nchini Israeli.
Iran nayo imeapa kuendelea kuwaunga mkono waasi hao ambao pia wanawaunga mkono wapiganaji wa kundi la Hamas kwenye mamlaka ya Palestina.
Mashambulio yaliyotekelezwa na ndege za kivita za Marekani na Uingereza, zililenga ngome 16 za waasi wa Houthi, ikiwemo ngome yake kuu na kuharibu silaha zake.
Rais Joe Biden amesema kitendo hicho kitasaidia, kulinda meli zinazotumia Bahari hiyo ili kuendeleza biashara za Kimataifa, huku Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akisema, ilikuwa muhimu kutekeleza mashambulio hayo kwa ajili ya kujilinda.