Maafisa katika eneo la Gaza inayoendeshwa na Hamas walisema siku ya Jumatatu makumi ya watu waliuawa usiku kucha katika mashambulizi “makali” ya Israel, wakati vita ambavyo vimeleta mshtuko katika eneo hilo vikipita hatua mbaya ya siku 100.
Ghasia mbaya katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel na mpaka wa Israel na Lebanon pamoja na mapigano kati ya wanajeshi wa Marekani na waasi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran katika Bahari Nyekundu yameibua hofu ya kuongezeka zaidi ya Ukanda wa Gaza.
Vita hivyo vilivyochochewa na mashambulio ya Wapalestina dhidi ya Israel, vimesababisha janga la kibinadamu kwa watu milioni 2.4 katika ukanda huo uliozingirwa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yameonya, na kupunguza sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa kifusi.
Wizara ya afya huko Gaza, inayotawaliwa na Hamas tangu 2007, iliripoti zaidi ya “mashahidi” 60 na makumi ya wengine kujeruhiwa, katika kile ofisi ya vyombo vya habari vya kundi hilo ilieleza kuwa “mashambulio makali” na mizinga katika Gaza.