Maelfu ya wakulima wa Ujerumani, madereva na wafanyakazi wa kilimo wamekusanyika pamoja na matrekta na vifaa vingine vizito mbele ya lango mashuhuri la Brandenburg la Berlin kwa ajili ya maandamano mengine ya wakulima waliokasirishwa na mipango ya serikali ya kusitisha punguzo la kodi kwa dizeli.
Polisi siku ya Jumatatu walikadiria kuwa takriban matrekta 3,000 tayari yalikuwa yamewasili kwa maandamano na inakadiriwa 2,000 zaidi walikuwa njiani katika kilele cha maandamano yao ya wiki.
Katika wiki iliyopita, wakulima walizifunga barabara kuu na kupunguza kasi ya magari kote Ujerumani kufuatia maandamano yao, kwa nia ya kuishinikiza serikali ya Kansela Olaf Scholz kuachana kabisa na mpango wa kuondoa nafuu za kodi kwenye sekta ya kilimo.
Maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu iliyopita yameongeza shinikizo kwa serikali ya mseto ya Kansela Sholz ambayo bado inahangaika kutatua mzozo kuhusu bajeti ya mwaka ujao.
Watu wapatao 10,000 wengi wakiwa ni wakulima wamehudhuria.