Rais anayemaliza muda wake wa Liberia George Weah amesema hana mpango wa kutaka kuchaguliwa tena mwaka 2029 baada ya kushindwa katika chaguzi za hivi karibuni.
Rais Weah, mwanasoka wa zamani wa kimataifa, alichaguliwa mwaka wa 2017 lakini akashindwa katika kura za Novemba na Joseph Boakai, ambaye anatazamiwa kuapishwa Jumatatu.
Akihutubia waumini wa kanisa hilo Jumapili viungani mwa mji mkuu, Monrovia, Bw Weah alisema atakuwa na umri wa miaka 63 baada ya miaka sita, na hatakuwa tayari kujihusisha na siasa zaidi ya miaka 65.
“Nina miaka 57 sasa na umri wetu wa kustaafu ni miaka 65 na miaka sita kuanzia sasa nitakuwa 63 na siwezi kufanya kazi kwa miaka miwili,” alisema.
Weah alisema “nahitaji wakati kwa ajili yangu, watoto na familia”.
“Sikuja kwenye siasa ili kuteka mamlaka. Hamtanivuta kwenye siasa hadi nifikishe miaka 90,” aliongeza.
“Nasema asanteni Waliberia kwamba nimekuwa rais iwe mara moja au mara 50, lakini ninaweza kuwahakikishia kuwa ni mara moja.”