Maafisa wa Afya nchini China wametahadharisha juu ya uwezekano wa kuibuka tena mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 katika mwezi huu wa Januari, utakaochochewa na kuongezeka maambukizi ya spishi mpya ya JN.1.
Ingawa kesi za maambukizi zilizopo hivi sasa ni za kiwango cha chini, na kiwango cha vipimo vilivyofanywa katika vituo vya uchunguzi ni chini ya asilimia moja, Tume ya Taifa ya Afya ya China (NHC) imetoa indhari ya ongezeko la uwepo wa spishi hiyo ya JN.1.
Wang Dayan, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Mafua cha China, ameeleza katika mkutano wa waandishi wa habari wa NHC ya kwamba, wataalamu wamefikia hitimisho kuwa aina mbalimbali za magonjwa ya kupumua zitaenea wakati wa majira ya baridi na msimu wa mapukutiko wa mwaka huu, na kati yao, virusi vya mafua itakuwa sababu kuu ya maradhi hayo.