Jeshi la Rwanda, limethibitisha kumuua mwanajeshi mmoja wa DRC na kuwakamata wengine wawili, baada ya kuvuka mpaka wao na kuingia nchini humo kwenye mpaka wa wilaya ya Rubavu usiku wa kuamkia leo.
Nchi ya DRC bado haijasema chochote kuhusiana na tukio hilo, ingawa miaka ya hivi karibuni, mataifa hayo mawili jirani yamekuwa katika mzozo, ambapo kwa mujibu wa umoja wa Mataifa, mgogoro wao unatishia kutokea vita.
Kinshasa imekuwa ikiituhumu Kigali kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa kutekeleza mashambulio katika eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Licha ya baadhi ya mataifa ya Magharibi ikiwemo Marekani kuitaka Kigali kuacha kuwaunga mkono waasi wa M23, Rwanda kwa upande wake imeendelea kukana tuhuma kuwa inawaunga mkono na kuwafadhili waasi hao.