Serikali za Tanzania na Angola zimesaini hati tatu za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, kuondoa visa kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba, Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Balozi Téte António wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Angola uliomalizika jana Visiwani Zanzibar.
Viongozi hao pia wamekubaliana kuyafanyia kazi masuala mbalimbali hususan kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda, kuandaa kongamano la bishara na uwekezaji, na kuziwezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja.