Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) kwa mara nyingine tena ametoa mwito wa kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza kwa misingi ya ubinadamu.
Moussa Fakki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU alitoa mwito huo jana Jumanne katika hotuba yake mbele ya Bunge la Nchi za Afrika na kuongeza kuwa, Wapalestina wasio na hatia ndio wanaolipa gharama kubwa na kupitia machungu, mateso na mauaji kwenye mgogoro huo.
Ameonya kuhusu mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, huku akikosoa vikali upuuzaji wa sheria za kimataifa katika mgogoro huo.
Mahamat amebainisha kuwa: Kuwashambulia kwa mabomu raia wa Kipalestina, uharibifu wa kimpangilio wa maisha yao, pamoja na kudunisha vifo, majanga yote haya yameendelea kwa zaidi ya siku 100.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Umoja wa Afrika pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, na hasa mataifa makubwa yenye nguvu duniani, kubeba jukumu la kusitisha mgogoro huo.