Nyota wa soka wa Ufaransa Karim Benzema amewasilisha kesi ya kuharibiwa jina dhidi ya waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa kwa kumtuhumu kuwa na uhusiano na Muslim Brotherhood, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.
Gérald Darmanin alisema mnamo Oktoba kwamba Bw Benzema “ana uhusiano mbaya” na kundi la Kiislamu la Sunni.
Maoni hayo “yanadhoofisha” heshima na sifa yake, wakili wa Bw Benzema alisema.
Kundi la Muslim Brotherhood limepigwa marufuku katika nchi kadhaa zikiwemo Misri, Urusi na Saudi Arabia.
Maoni ya Darmanin mwezi Oktoba yalikuja baada ya mchezaji huyo kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa anaunga mkono watu wa Gaza kama “waathiriwa tena wa mashambulizi ya kidhalimu ya mabomu ambayo hayawaachi wanawake wala watoto”.
Akibainisha kushindwa kwake kuonesha huruma kama hiyo kwa wahanga 1,300 wa Israel waliouawa na Hamas tarehe 7 Oktoba, Bw Darmanin alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Ufaransa “anajulikana sana kwa uhusiano wake na Muslim Brotherhood”.
“Tunapambana na zimwi ambalo ni Muslim Brotherhood, kwa sababu inajenga mazingira ya jihadi,” mwanasiasa huyo alikiambia kituo cha televisheni cha kihafidhina cha CNews.