Upinzani usio na silaha nchini Chad siku ya Jumatano umemtaka rais wa mpito Jenerali Mahamat Idriss Déby Itno, ambaye alichukua mamlaka kufuatia kifo cha babake mwaka 2021, kuacha kugombea katika uchaguzi ujao wa urais, uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2024.
Jukwaa kuu la upinzani na mashirika ya kiraia, Wakit Tamma, wanashutumu “jumuiya ya kimataifa”, hususan Ufaransa, kwa kuunga mkono “mrithi wa kifalme” katika uongozi wa nchi hii ya Sahel na kumuongezea nguvu Mahamat Déby katika ” nia yake ya kumiliki utawala, ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu.
Akiwa na umri wa miaka 37, Mahamat Déby alitangazwa na jeshi mnamo Aprili 20, 2021 kuwa rais wa mpito akiwa mkuu wa utawala wa kijeshi unaoongozwa na majenerali 15, baada ya kifo cha baba yake Idriss Déby Itno aliyeuawa na waasi alipokuwa akielekea kwenye uwanja wa vita. Alitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 30 baada ya kuchukua mamlaka kufuatia mapinduzi ya kijeshi.